Jun 15, 2019 03:53 UTC
  • Magaidi wa Daesh wadai kuua makumi ya askari nchini Nigeria

Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika eneo la Magharibi mwa Afrika (ISWA) limedai kwamba limeua makumi ya askari wa Nigeria huko kaskazini mwa nchi hiyo.

Tovuti ya SITE Intelligence imelinukuu genge hilo la ukufurishaji likidai kuwa, wanachama wake wameua wanajeshi 20 baada ya kuvamia kambi moja ya jeshi katika mji wa Kareto, katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.

Duru za kiusalama pia zimekiri kuwa, kambi hiyo ya Kikosi cha 158 cha jeshi la Nigeria iliyoko yapata kilomita 130 kutokana mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo hilo ilishambuliwa alfajiri ya Alkhamisi na kwamba kamanda mmoja wa ngazi za juu ni miongoni mwa askari waliouawa.  

Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) katika eneo la Magharibi mwa Afrika (ISWA) ambalo lilijitenga na genge la kitakfiri la Boko Haram mwaka 2016 limetekeleza wimbi la mashambulizi dhidi ya raia na maafisa usalama nchini Nigeria katika miezi ya hivi karibuni.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wanajeshi wasiopungua 17 na raia tisa kuuawa katika shambulio lililofanywa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram huko Darak, kaskazini mwa Cameroon.

Ramani inayoonyesha jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria

Kundi hilo mwaka 2009 lilishika silaha na kuanzisha mashambulizi na hujuma kaskazini mwa Nigeria na kisha kujipenyeza pia katika nchi jirani  za Niger, Chad, na kaskazini mwa Cameroon.

Tangu wakati huo hadi sasa, kundi la kigaidi la Boko Haram limeuwa watu zaidi ya elfu 20 katika nchi hizo na kuwafanya wengine zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi. 

Tags