Jun 24, 2019 12:42 UTC
  • Askari 11 wa Chad wauawa katika shambulizi la Boko Haram Ziwa Chad

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limeua askari 11 wa Chad, katika eneo la Ziwa Chad.

Maafisa wa serikali katika eneo hilo wameviambia vyombo vya habari kuwa, askari hao wa Chad wakiwemo maafisa usalama watatu na wanajeshi sita wameuawa katika hujuma mpya ya Boko Haram katika mji wa Mbomouga, eneo la Ngouboua linalopakana na Ziwa Chad.

Taarifa ya Jumapili ya maafisa hao imeongeza kuwa, wanachama 26 wa Boko Haram wamengamizwa pia katika makabiliano hayo. Duru za kiusalama zinasema wapiganaji hao wa Boko Haram waliouawa walikuwa wameiba mifugo ya wakazi wa eneo hilo.

Shambulizi hilo la Boko Haram linajiri siku chache baada ya Kikosi cha Pamoja cha Nchi Zinazopakana na Ziwa Chad (MNJTF) kufanikiwa kuangamiza makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika kisiwa cha Doron Naira katika eneo hilo la Ziwa Chad.

Askari wa Kikosi cha Pamoja cha Nchi Zinazopakana na Ziwa Chad

Taarifa iliyotolewa na kikosi hicho imesema kuwa, magaidi 42 waliuawa katika operesheni ya Ijumaa, na kwamba kikosi hicho kimepoteza askari mmoja tu katika makabiliano hayo na magaidi wa Daesh, huku wanajeshi wengine 10 wakijeruhiwa.

Hata hivyo Kundi la Kigaidi la Daesh Magharibi mwa Afrika (ISWAP) ambalo lilijiondoa kwenye genge la Boko Haram na kutangaza utiifu wake kwa ISIS mwaka 2016 limedai kuwa limeua wanajeshi 15 wa Kikosi cha Pamoja cha Nchi Zinazopakana na Ziwa Chad katika mapigano hayo ya Juni 21 katika mji wa Garno, jimboni Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria, mpakani na Ziwa Chad.

Tags