Wapinzani Algeria waafiki kwa mara ya kwanza mpango wa serikali ya muda
Wapinzani nchini Algeria wamekubali katika mkutano wa mazungumzo yao ya kitaifa kuhusu mpango wa serikali na kuweka masharti katika uwanja huo.
Mkutano wa mazungumzo ya kitaifa ya wapinzani nchini Algeria ulifanyika jana Jumamosi na washiriki walisisitiza katika taarifa ya mwisho ya mkutano huo kuhusu udharura wa kufukuzwa maafisa wote waliohusika katika ufisadi na udanganyifu wakati wa uchaguzi wa duru iliyopita nchini humo.
Wapinzani hao wamesisitiza kuwa wanapinga serikali kuunda tume huru kuu ya uchaguzi na wametaka kuundwa kamati ya kitaifa. Wapinzani hao wa Algeria kupitia taarifa yao hiyo wameafiki ombi la Rais wa muda wa nchi hiyo Abdulqadir bin Saleh kwa ajili ya kufanya mazungumzo. Bin Saleh hivi karibuni alitoa wito wa kufanyika mazungumzo ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Algeria pasina uingiliaji wa serikali au jeshi.
Wananchi wa Algeria wanasisitiza kuwa taasisi na shakhsia waliokuwa madarakani wakati wa utawala wa Rais aliyepinduliwa Abdelaziz Bouteflika hawapasi kukabidhiwa nyadhifa za kuongoza kipindi cha mpito. Wananchi hao kila wiki siku ya Ijumaa hufanya maandamano kutilia mkazo takwa lao hilo. Maelfu ya wananchi wa Algeria Ijumaa ya juzi pia walifanya maandamano kwa mara ya ishirini baada ya Sala ya Ijumaa huku usalama ukiwa umeimarishwa vikali. Bouteflika alijiuzulu mwezi Mei mwaka huu baada ya kusalia madarakani kwa miaka ishirini. Alichukua hatua hiyo baada ya kukabiliwa na mashinikizo na maandamano makubwa ya wananchi.