Jeshi la Nigeria laendelea kuwashambulia wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54729-jeshi_la_nigeria_laendelea_kuwashambulia_wafuasi_wa_sheikh_ibrahim_zakzaky
Vikosi vya usalama nchini Nigeria vimetumia risasi za vita dhidi ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo, waliomiminika barabarani jana Ijumaa kwa lengo la kushinikiza kuachiliwa kwake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 13, 2019 03:00 UTC
  • Jeshi la Nigeria laendelea kuwashambulia wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky

Vikosi vya usalama nchini Nigeria vimetumia risasi za vita dhidi ya wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo, waliomiminika barabarani jana Ijumaa kwa lengo la kushinikiza kuachiliwa kwake.

Wafuasi wa kiongozi huyo walifanya maandamano ya amani mjini Kaduna jana Ijumaa wakiitaka serikali ya nchi hiyo kumuachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, ambapo hata hivyo walifyatuliwa risasi hai. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa serikali ya Nigeria wamejizuia kutangaza idadi ya watu waliofariki au kujeruhiwa kufuatia shambulizi hilo. Maafisa usalama wa Nigeria pia wamewatia mbaroni wafuasi kadhaa wa kiongozi huyo wa kidini mjini Abuja.

Maandamano ya Waislamu wa Nigeria

Kwa mujibu wa habari hiyo, kwa akali watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi katika maandamano ya siku ya Jumanne yaliyofanyika mbele ya bunge la nchi hiyo. Ikumbukwe kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria alikamtwa baada ya kupigwa risasi na kujeruhiwa vibaya yeye na mke wake mwezi Disemba 2015 wakati jeshi la nchi hiyo lilipovamia Husainia ya Baqiyyatullah mjini Zaria na kuua kwa umati mamia ya Waislamu. Hii ni katika hali ambayo hali ya kiafya ya shakhsia huyo inaarifiwa kuendelea kuwa mbaya kila siku. Licha ya mahakama ya nchi hiyo kuitaka serikali kumuachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, lakini bado anaendelea kushikiliwa katika korokoro za serikali hadi sasa.