Wanigeria waendeleza maandamano ya kutaka kuachiwa huru Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54876-wanigeria_waendeleza_maandamano_ya_kutaka_kuachiwa_huru_zakzaky
Waislamu na wanaharakati nchini Nigeria jana Ijumaa waliendeleza maandamano ya kutaka kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo licha ya kukabiliwa kwa mkono wa chuma na maafisa usalama wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 20, 2019 02:59 UTC
  • Wanigeria waendeleza maandamano ya kutaka kuachiwa huru Zakzaky

Waislamu na wanaharakati nchini Nigeria jana Ijumaa waliendeleza maandamano ya kutaka kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo licha ya kukabiliwa kwa mkono wa chuma na maafisa usalama wa nchi hiyo.

Maandamano makubwa ya amani yalishuhudiwa jana katika jimbo la Katsina, kaskazini magharibi mwa nchi, ambapo waandamanaji wameiomba mahakama iruhusu Sheikh Zakzaky na mkewe waende wakatibiwe nje ya nchi.

Haya yanajiri katika hali ambayo, duru za kieneo zimetangaza kuwa, Mahakama Kuu ya Nigeria inachunguza uwezekano wa kuruhusiwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kwenda kutibiwa nchini India.

Wanaharakati wa mitandao ya kijamii nchini Nigeria jana Ijumaa walisambaza picha zinazoonesha Sheikh Zakzaky na mkewe wakiwa wamefungiwa katika chumba kimoja sehemu isiyojulikana.

Siku chache zilizopita, mtu mmoja aliuawa na maafisa usalama katika mji wa Kano nchini Nigeria wakati wa maandamano makubwa ya kushinikiza kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Sheikh Zakzaky na mkewe wakiwa wamefungiwa katika chumba kimoja sehemu isiyojulikana.

Mauaji hayo yalifanyika chini ya wiki moja baada ya maafisa usalama wa nchi hiyo kutumia risasi hai na mabomu ya kutoa machozi kuvunja maandamano mengine ya amani ya wananchi katika miji ya Kano,  Abuja na Kaduna, ambapo watu watatu akiwemo mtoto mdogo waliuawa.

Sheikh Zakzaky na mkewe walitiwa mbaroni tarehe 13 Disemba 2015 katika Huseiniya ya Harakati ya Kiislamu huko Zaria kufuatia shambulio la jeshi la nchi hiyo lililoua shahidi mamia ya Waislamu wasio na hatia, na serikali imepuuza agizo lilitolewa na Mahakama Kuu ya nchi hiyo mwaka 2016 la kutaka msomi huyo wa Kiislamu aachiwe huru.