Watu 6 wauliwa na genge lenye silaha kusini mwa Niger
Viongozi wa Niger wamethibitisha habari ya kuuawa watu sita katika shambulio la genge moja lenye silaha kusini mwa nchi hiyo katika mpaka wake na Nigeria.
Viongozi wa Niger wamesema kuwa, shambulizi la kundi moja lenye silaha lililofanyika karibu na mji wa Madarounfa katika jimbo la Maradi la kuisni mwa Niger, limeua raia sita na kujeruhi wengine kadhaa.
Viongozi hao wameongeza kuwa, genge moja la watu wenye silaha limevuka mpaka kutokea Nigeria na kufanya shambulio hilo dhidi ya raia ambapo mbali na kuua na kujeruhi raia hao, limewapora pia mali zao.
Kwa miezi kadhaa sasa jimbo la Maradi lililoko katika mpaka wa Niger na Nigeria limekuwa ni maficho ya magenge ya wahalifu ambao mara kwa mara hufanya uporaji na kuua raia. Si hayo tu, lakini pia tangu mwezi Januari mwaka huu hadi hivi sasa, karibu wanajeshi 10 wa Niger wameshauawa katika mashambulio tofauti ya magenge hayo.
Wakazi wa pande mbili za mpaka wa pamoja wa Niger na Nigeria kila leo wanakumbwa na vitendo vya uhalifu kutoka kwa magenge yenye silaha kama vile mauaji, wizi, ujambazi na utekaji nyara watu.
Hii ni katika hali ambayo hivi sasa kuna wakimbizi zaidi ya 20 elfu waliokimbia vijiji vyao nchini Niger kutoka na vitendo vya uhalifu katika maeneo yao. Wengi wa wakimbizi hao wamekimbilia mjini Maradi.
Genge la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram lenye makao yake makuu nchini Nigeria limewasababishia matatizo makubwa raia wa nchi hizo mbili wakiwemo wale wa jimbo la Diffa, la kusini mashariki mwa Niger, karibu na mpaka wa nchi hiyoi na Nigeria.