Uganda yaanza jaribio kubwa zaidi la utoaji chanjo ya Ebola
Uganda imeanza jaribio kubwa zaidi la utoaji wa chanjo dhidi ya homa hatari ya Ebola kufuatia kuwepo wasiwasi wa kuenea pakubwa maambukizo ya ugonjwa huo kutokea katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Uganda imekuwa katika hali ya tahadhari kubwa tangu kuripotiwa kuaga dunia kwa ugonjwa huo watu wawili wa familia moja ambao walikuwa safarini nchini Uganda wakitokea Kongo. Mtu wa tatu wa familia hiyo pia aliaga dunia baada ya kurejea nyumbani.
Ugonjwa unaombukiza kwa kasi wa Ebola hadi sasa umeuwa watu zaidi ya 1,800 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mlipuko wa maradhi hayo ulioiathiri nchi hiyo ya katikati mwa Afrika hivi karibuni. Si Kongo pekee, nchi ya Rwanda ambayo ni jirani ya Kongo na Uganda imechukua hatua za tahadhari baada ugonjwa huo kuenea katika mji wa Goma nchini Kongo. Mji wa Goma unatambulika kama kito cha biashara karibu na mpaka wa nchi mbili hizo.
Pontiano Kaleebu Mtafiti Mwandamizi anayeongoza mradi wa utoaji chanjo hiyo huko Uganda amesema kuwa zoezi hilo litakalodumu kwa miaka miwili litawashirikisha watu 800 katika wilaya ya Mbarara kusini magharibi mwa nchi hiyo. Aidha chanjo hiyo itatolewa kwa kushirikiana watafiti wa Uganda na wale wa kimataifa kwa kuungwa mkono na London School of Hygiene and Tropical Medicine.