HRW yakosoa ukandamizaji wa Saudia dhidi ya wahajiri wa Kiethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55423-hrw_yakosoa_ukandamizaji_wa_saudia_dhidi_ya_wahajiri_wa_kiethiopia
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeeleza wasiwasi wake kuhusu haki ya wahajiri wa Kiethiopia nchini Saudi Arabia na kukosoa ukiukwaji wa haki zao unaofanywa na maafisa wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 16, 2019 23:12 UTC
  • HRW yakosoa ukandamizaji wa Saudia dhidi ya wahajiri wa Kiethiopia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limeeleza wasiwasi wake kuhusu haki ya wahajiri wa Kiethiopia nchini Saudi Arabia na kukosoa ukiukwaji wa haki zao unaofanywa na maafisa wa nchi hiyo.

Ripoti iliyotolewa na Human Rights Watch imelaani vikali mienendo ya maafisa wa Saudi Arabia dhidi ya wahajiri wa Kiethiopia ikiwa ni pamoja na mateso, kunyanyaswa, kufungwa katika mazingira mabaya na hata kuuliwa. 

Ripoti hiyo ambayo imetegemea ushahidi wa baadhi ya wahajiri hao imesema kuwa: Askari walinzi wa mipaka wa Saudia hawasiti kuwafyatulia risasi wahajiri wa Kiethiopia kwa kadiri kwamba, baadhi ya wahajiri hao wameuawa na wengine wamejeruhiwa. 

Wahajiri wa Kiethiopia wananyanyaswa Saudia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limenukuu ripoti ya Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) na kusema: Tangu mwezi Mei mwaka 2017 hadi Machi mwaka huu maafisa wa Saudi Arabia waliwakamata na kuwafukuza nchini humo raia 260 wa Ethiopia na mwenendo huo unaendelea. 

Shirika hilo limewalaumu maafisa wa nchi mbili za Saudia na Ethiopia kwa kutochukua hatua za lazima za kukomesha ukatili huo. 

Shirika la Kimataifa la Wahajiri linasema kuwa, wahajiri wa Kiethiopia wanakabiliana na mashaka na hatari nyingi wakiwa baharini kuelekea Saudi Arabia na baada ya kuwasili nchini humo hukamatwa na kufungwa katika mazingira mabaya sana ambako huteswa na kunyanyaswa na kisha hufukuzwa nchini humo.