Duru za habari: Sheikh Zakzaky huenda akazuiwa kutoka nje ya nchi
Duru za ndani ya Nigeria zimeripoti kuwa, serikali ya nchi hiyo huenda ikamzuia kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN), Sheikh Ibrahim Zakzaky kwenda nje ya nchi hiyo.
Ripoti zinasema kuwa, Serikali ya Federali ya Nigeria yumkini ikamzuia Sheikh Zakzaky kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Habari hiyo imethibitishwa na afisa mmoja wa ngazi za juu wa vyombo vya usalama vya serikali ya Nigeria. Afisa huyo amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba, serikali haitampatia tena Sheikh Zakzaky ruhusa ya kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, hata kama ruhusa hiyo itatolewa na mahakama.
Wakati huo huo Katibu wa Wizara ya Habari na Utamaduni ya Nigeria ametoa taarifa akidai kuwa, katika safari yake nchini India, Sheikh Zakzaky aliwasiliana na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kama Kamisheni ya Kiislamu ya Haki Binadamu kwa ajili ya kupewa ukimbizi nje ya Nigeria.
Hata hivyo madai hayo yamekadhibishwa na Msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Ibrahim Mussa ambaye amesema serikali ya Abuja inaeneza uongo dhidi ya Sheikh Zakzaky.
Vilevile wakili wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Femi Falana amekadhibisha madai hayo na kuitaka serikali ya Nigeria kumpa huduma za tiba msomi huyo na mke wake.
Alkhamisi iliyopita Sheikh Zakzaky alilazimika kuondoka New Delhi India alikokuwa amefika siku chache kabla kupata matibabu. Sheikh Zakzaky amechukua uamuzi huo kutokana na kutoridhika na mchakato mzima wa matibabu pamoja na vizingiti vya usalama alivyowekewa sambamba na kunyimwa ruhusha madakatari wake anaowaamini kumtibu.