Magufuli ahitimisha mkutano wa viongozi wa SADC, Dar
(last modified Sun, 18 Aug 2019 12:05:47 GMT )
Aug 18, 2019 12:05 UTC
  • Magufuli ahitimisha mkutano wa viongozi wa SADC, Dar

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambaye ni Rais wa Tanzania, John Magufuli leo amefunga Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kabla ya kuhitimishwa mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi hizo, Rais Magufuli amesema wameagiza Sekretarieti kuanzisha chombo cha kukabiliana na majanga ili kuzisaidia nchi wanachama zitakapokumbwa na mafuriko, njaa na magonjwa ya milipuko.

Amesema pia kwamba wameagiza Burundi iliyoomba kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo kukamilisha hatua kadhaa kabla kupewa uanachama.

Katika mkutani wa Sadc wa Dar es Salaam kumesainiwa itifaki kuhusu maendeleo ya viwanda, kubadilishana watuhumiwa na wafungwa na masuala ya jinai.

Tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo mwaka 1992, itifaki 33 zimeshasainiwa na wakuu wa nchi hizo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) pia ametangaza Kiswahili kuwa lugha ya nne itakayotumika katika nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo.

Mkutano wa SADC, Dar es Salaam

Siku nne zilizopita baraza la mawaziri la jumuiya hiyo lilipitisha pendekezo kuwa Kiswahili kianze kutumika kama lugha ya nne pamoja na kuwasilisha hoja nyingine 107 ili kujadiliwa.

Magufuli amesema katika kikao kilichofanyika jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakuu hao kwa pamoja wamekubaliana lugha hiyo ianze kutumika.

Lugha zilizokuwa zikitumika katika nchi hizo 16 ni Kiingereza, Kireno na Kifaransa.  Kuanzia sasa Kiswahili kitatumika katika mikutano ya jumuiya hiyo pamoja na machapisho yake mbalimbali.