Mwito wa Umoja wa Mataifa kwa serikali ya Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5560-mwito_wa_umoja_wa_mataifa_kwa_serikali_ya_myanmar
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon amemtaka mjumbe maalumu wa umoja huo nchini Myanmar atafute njia za kutatua mgogoro wa Waislamu wa kabila la Rohingya na kuwaondolea masaibu yao, baada ya kufa maji - siku chache zilizopita - makumi ya Waislamu hao kutokana na mateso wanayofanyiwa na mabudha wenye chuki kali za kidini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 22, 2016 00:08 UTC
  • Mwito wa Umoja wa Mataifa kwa serikali ya Myanmar

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki moon amemtaka mjumbe maalumu wa umoja huo nchini Myanmar atafute njia za kutatua mgogoro wa Waislamu wa kabila la Rohingya na kuwaondolea masaibu yao, baada ya kufa maji - siku chache zilizopita - makumi ya Waislamu hao kutokana na mateso wanayofanyiwa na mabudha wenye chuki kali za kidini.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Waislamu wasiopungua 21 wakiwemo watoto wadogo walipoteza maisha siku ya Jumanne baada ya boti yao kuzamishwa na mawimbi makali ya baharini. Msemaji wa ofisi ya uratibu wa masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ya huko Yangon, mji mkuu wa kibiashara wa Myanmar amesema kuwa, Waislamu hao wamepoteza maisha huko Sittwe, makao makuu ya jimbo la Rakhine lenye Waislamu wengi wa kabila la Rohingya. Mmoma wa wanaharakati wa Kiislamu wa kabila la Rohingya ameuambia Umoja wa Mataifa kuwa vifo hivyo vimetokea kutokana na hali mbaya mno wanayoishi nayo wislamu wa kabila la Rohingya kwani Waislamu hao wamepigwa marufuku hata kutumia vyombo vya usafiri wa umma hivyo wanalazimika kutumia njia za hatari kwa ajili ya kazi zao za lazima kama vile kwenda maeneo ya mbali kununua madawa na mahitaji yao ya lazima. Si hayo tu, lakini pia Waislamu wa kabila la Rohingya wanabanwa sana na viongozi wa Myanmar ambao ni mabudha wanaodhibiti kila kitu nchini humo. Hivi sasa kuna kambi kadhaa za wakimbizi wa Rohingya huko Rakhine, magharibi mwa Myanmar, na Waislamu waliorundikwa kwenye kambi hizo wanaishi katika mazingira magumu mno. Serikali ya Myanmar inaendelea kupinga haki ya uraia ya Waislamu hao na inadai kuwa Waislamu hao ni wageni waliohamia nchini Myanmar kutokea Bangladesh. Lakini Waislamu wa Rohingya wanakanusha vikali madai hayo wakisema kuwa, wao si wageni, bali ni raia wenye wa asili na jadi wa Myanmar. Waandishi wa habari waliopata fursa ya kutembelea maeneo ya Waislamu hao wanasema kuwa, Waislamu hao wa Rohingya wanaishi katika mazingira magumu mno katika kambi hizo na kusisitiza kuwa, ubaguzi wa kuchupa mipaka wanaofayiwa Waislamu hao, hauvumiliki. Amma msimamo uliochukuliwa na mkuu wa chama tawala nchini Myanmar, Aung San Suu Kyi, unaonesha ni muelekeo gani inaelekea serikali mpya ya Myanmar. Mwaka 2012 zaidi ya Waislamu elfu moja waliuliwa kinyama na kikatili na mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka, na zaidi ya laki moja wengine wakalazimika kukimbia makazi yao, Bi Aung San Suu Kyi hajachukua msimamo wowote wa maana wa kuwatetea Waislamu hao wanaodhulumiwa, na wala hajalaani uvunjaji huo mkubwa wa haki za binadamu. Suala hilo liliyavunja moyo sana mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani hasa kwa kuzingatia kuwa, Aung San Suu Kyi ni mshindi wa tunzo ya amani ya Noble na mwenyewe amekuwa akidai kuwa ni mpiganiaji mkubwa wa amani na haki za binadamu. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, Aung San Suu Kyi alijifanya ni mpiganiaji amani na usalama duniani ili apate uungaji mkono wa kimataifa tu. Kwani hivi sasa ana nguvu za kutosha za kuweza kuzuia mateso na masaibu wanayoyapata Waislamu huko Myanmar, lakini hafanyi chochote cha kuwasaidia. Hivi sasa pia jamii ya kimataifa inasubiri kuona Aung San Suu Kyi atachukua hatua gani kufuatia kufa maji zaidi ya Waislamu 20 wanaondelea kuteswa kwa kila namna na mabudha wenye taasubu na chuki kubwa za kidini.