Kenya ina idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56480-kenya_ina_idadi_kubwa_ya_watumiaji_wa_dawa_za_kulevya
Wizara ya Afya ya Kenya imeripoti kuwa nchi hiyo inaendelea kushuhudia watumiaji wengi za madawa ya kulevya.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Oct 08, 2019 00:59 UTC
  • Kenya ina idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya

Wizara ya Afya ya Kenya imeripoti kuwa nchi hiyo inaendelea kushuhudia watumiaji wengi za madawa ya kulevya.

Idadi ya watu wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 katika kipindi cha miaka minane iliyopita; wengi wao wakijidunga dawa aina ya heroini. Mwananchi wa Kenya kwa jina la Peter ambaye hivi sasa ameacha kutumia dawa hizo za kulevya amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa anatamani asahau kabisa uraibu aliokuwa nako kwa miaka 14 iliyopita. Peter hivi sasa anatumia dawa aina ya methadone kama msaada ili kuweza kurejea katika hali ya kawaida baada ya kuacha kutumia dawa za kulevya aina ya heroini.  Dozi moja ya heroini inauzwa kwa shilingi 150 za Kenya. Hayo yameelezwa na watumiaji wa mihadarati hiyo ambayo hivi sasa wameacha.

David Ndegwa Mkurugenzi wa Afya katika Kaunti ya Kiambu ambako Jumuiya ya Madaktari wasio na Mipaka (MSF) mwezi huu ilifungua kliniki umbali wa kilomita 20 kaskazini mwa mji mkuu Nairobi amesema kuwa vijana wadogo katika matabaka mbalimbali ya jamii wanatumia njia ya kujidunga sindano za heroini.

Mji wa Mombasa

Inafaa kuashiria hapa kuwa, dawa za kulevya aina ya heroini huingizwa nchini Kenya kupitia mji wa bandari wa Mombasa ambao ni kitovu kinachokuwa cha upokeaji wa mihadarati kutoka nchini Afghanistan kuelekea nchi za Magharibi.  Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayohusika Mihadarati na Jinai imesema katika ripoti yake kuwa, bara la Afrika kuanzia mwaka 2006 hadi 2016 lilikuwa linaongoza kwa kuwa na ongezeko la kasi la watumiaji wa heroini.

Kliniki hiyo iliyofunguliwa na Jumuiya ya MSF ni ya kwanza nchini Kenya kwa ajili ya kutoa matibabu ya methadone kwa watumiaji ya heroini pamoja na huduma nyingine muhimu.