5 wauawa katika maandamano ya wapinzani wa Rais Conde wa Guinea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56644-5_wauawa_katika_maandamano_ya_wapinzani_wa_rais_conde_wa_guinea
Watu watano wameripotiwa kuuawa katika ghasia za maandamano ya wapinzani wanaopinga uwezekano wa Rais Alpha Conde wa Guinea kugombea muhula wa tatu wa urais kinyume na katiba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2019 23:24 UTC
  • 5 wauawa katika maandamano ya wapinzani wa Rais Conde wa Guinea

Watu watano wameripotiwa kuuawa katika ghasia za maandamano ya wapinzani wanaopinga uwezekano wa Rais Alpha Conde wa Guinea kugombea muhula wa tatu wa urais kinyume na katiba.

Waandamanaji hao wanasema serikali inapika njama ya kuifanyia katiba marekebisho, ili kutoa mwanya kwa Rais Conde kuwania muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu ujao.

Maandamano hayo yalianza siku ya Jumatatu. Maafisa wa polisi wamezingira makazi ya viongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Union of Republican Forces (UFR), Cellou Dalein Diallo na Sidya Toure. Cellou Dalein Diallo, Waziri Mkuu wa zamani nchini humo amekuwa akiongoza upinzani dhidi ya Rais Alpha Condé.

Rais Alpha Conde wa Guinea 

Licha ya maafisa usalama kutumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano hayo, lakini wafuasi hao wa upinzani wameapa kuendeleza maandamano hayo hadi pale Rais Conde atakapotupilia mbali mpango huo wa kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi ujao mwakani.

Mwezi uliopita, Rais Conde mwenye umri wa miaka 81 aliliambia taifa hilo lijiandae kwa kura ya maoni, bila kutoa maelezo zaidi. Kwa mujibu wa wapinzani nchini humo, tangu alipoingia madarakani Rais Alpha Condé wa nchi hiyo hapo mwaka 2010, maafisa usalama wameshawaua mamia ya waandamanaji wanaopinga siasa za rais huyo.