Mgomo na maandamano Kenya kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta
-
Maandamano Nairobi, Kenya kufuatia kupanda kwa bei ya Mafuta, 18 Mei 2026
Maandamano dhidi ya kupanda kwa bei ya mafuta yamezuka katika miji kadhaa nchini Kenya siku ya Jumatatu huku athari mbaya za vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran zikiendelea kuhisika duniani kote.
Ongezeko hilo la bei ya petroli na dizeli imesababisha mgomo wa kitaifa wa sekta ya uchukuzi, hali iliyowaacha maelfu ya abiria wakiwa wamekwama na wengi kulazimika kutembea kwa miguu kuelekea katika maeneo yao ya kazi.
Muungano wa Sekta ya Uchukuzi Kenya ulitangaza Jumapili kuwa magari yote yatasitisha huduma kuanzia saa sita usiku wa kuamkia Jumatatu, kama ishara ya kupinga ongezeko la hivi punde la bei za mafuta. Kwa upande wake, jeshi la polisi lilisema kuwa litachukua hatua madhubuti kukabiliana na uvurugaji wowote wa amani.
Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Petroli ya Kenya (EPRA) wiki iliyopita ilipandisha bei ya rejareja ya mafuta kwa asilimia 23.5—hatua iliyofuatia ongezeko jingine la asilimia 24.2 mwezi uliopita. Hivyo basi, petroli sasa inauzwa Sh214.25 kwa lita na dizeli kwa Sh242.92, huku bei ya mafuta ya taa ikibaki Sh152.78. Hali hiyo inatokana na vita haramu vya Marekani na Israel dhidi ya Iran ambavyo vimevuruga usambazaji wa mafuta na gesi duniani.
Kufikia Jumatatu asubuhi, barabara kuu zinazoingia jijini Nairobi zilikuwa zimefungwa na waendeshaji wa vyombo vya usafiri waliokuwa kwenye mgomo, sambamba na makundi madogo ya waandamanaji. Polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi katika baadhi ya maeneo, huku baadhi ya waandamanaji wakichoma matairi kuziba barabara muhimu, hali iliyoongeza msongamano wa magari na kuwawia vigumu abiria kufika waendako.
Waziri wa Fedha, John Mbadi, akizungumza na kituo cha Citizen TV, alisema kuwa wizara za fedha na nishati zinatazamia kufanya mazungumzo na wadau wa uchukuzi ili kutafuta mwafaka, akibainisha kuwa bei za sasa tayari zimejumuisha ruzuku ya serikali.
Katibu Mkuu wa chama tawala cha UDA, Hassan Omar, kwa upande wake amesema kuwa hasira ya umma haipaswi kuelekezwa kwa serikali, bali inapaswa kuelekezwa kwa tawala za Marekani na Israel, ambazo ndizo zilizoanzisha vita dhidi ya Iran, hali ambayo imesababisha kuyumba kwa usambazaji wa mafuta duniani.