Wazimbabwe waandamana kupinga vikwazo vya nchi za Magharibi, wasema ni utumwa mamboleo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56849-wazimbabwe_waandamana_kupinga_vikwazo_vya_nchi_za_magharibi_wasema_ni_utumwa_mamboleo
Wafuasi wa chama tawala nchini Zimbabwe wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Harare wakilaani vikwazo vya nchi za Maghaibi ambavyo Rais Emmerson Mnangagwa wa nchi hiyo anasema vimedumaza uchumi wa Zimbabwe.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 25, 2019 13:05 UTC
  • Wazimbabwe waandamana kupinga vikwazo vya nchi za Magharibi, wasema ni utumwa mamboleo

Wafuasi wa chama tawala nchini Zimbabwe wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Harare wakilaani vikwazo vya nchi za Maghaibi ambavyo Rais Emmerson Mnangagwa wa nchi hiyo anasema vimedumaza uchumi wa Zimbabwe.

Mnangagwa kama akivyokuwa mtangulizi wake, Robert Mugabe, analaumu vikwazo vya kiuchumi vya nchi za magharibi dhidi ya Zimbabwe vinavyoendelea kwa miongo miwili sasa kuwa vimeharibu na kudumaza uchumi wa nchi hiyo.

Hata hivyo wapinzani wake wanasema anatumia kisingizio cha vikwazo kama njia ya kuficha kufeli kwa sera zake za kiuchumi.

Maandamano ya leo ya maelfu ya watu mjini Harare ambayo yameongozwa na mke wa Mnangagwa, Auxillia yamemalizikia kwenye uwanja wa taifa wa Harare ambako waandamanaji walionekana wakiimba na kucheza wakiwa na mabango yenye maandishi: "Hatutaki vikwazo na ubaguzi", "vikwazo ni aina mpya ya utumwa".

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ameitangaza leo Ijumaa kuwa ni likizo ya kitaifa na alitazamiwa kuhutubia umma kabla ya mechi ya mpira wa miguu baina ya timu mbili kubwa zaidi za soka nchini humo.

Rais Emmerson Mnangagwa

Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya zilikiwekea vikwazo chama tawala cha ZANU-PF na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Zimbabwe tangu mwaka 2001 kwa madai ya kukiuka haki za binadamu na kuchakachua uchaguzi. Hata hivyo serikali ya Harare inasema vikwazo hivyo ni fimbo ya adhabu ya Wamagharibi dhidi ya Zimbabwe baada ya nchi hiyo kutwaa mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na wazungu waliowachache.