Wakenya laki moja waishtaki Uingereza kutokana na jinai za ukoloni wake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56954-wakenya_laki_moja_waishtaki_uingereza_kutokana_na_jinai_za_ukoloni_wake
Zaidi ya Wakenya 100,000 wamewasilisha mashtaka kwa Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza kutokana na jinai ya kuwapora ardhi zao zenye rutuba na kuwapeleka sehemu kame.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 30, 2019 10:31 UTC
  • Wakenya laki moja waishtaki Uingereza kutokana na jinai za ukoloni wake

Zaidi ya Wakenya 100,000 wamewasilisha mashtaka kwa Umoja wa Mataifa dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza kutokana na jinai ya kuwapora ardhi zao zenye rutuba na kuwapeleka sehemu kame.

Waliowasilisha malalmiko ni wakaazi wa eneo la Kericho, magharibi mwa Kenya ambao walipokonywa ardhi zao zenye rotuba katika zama za ukoloni wa Muingereza. Ardhi hizo zilitumika kupanda chai ya mashirika makubwa ya Uingereza.

Kwa mujibu wa taarifa, mawakili leo Jumatano wametembelea eneo la Kericho ili kuandaa mashtaka dhidi ya serikali ya Uingereza wakitaka iwajibike kutokana na udhalimu waliotendewa Wakenya katika zama za ukoloni.

Mawakili hao pia wanalenga kuwasilisha mashtaka dhidi ya jeshi na makamanda wa dola la kiloloni la Uingereza kutokana na jinai zinazojumuisha mateso, mauaji, uteketezaji wa makusudi wa ardhi za kilimo za wenyeji wa eneo la Kericho sambamba na kukiuka haki zao za binadamu.

Mashamba ya Chai, Kericho Kenya

Mawakili hao wanasema, hadi sasa wakuu wa Uingereza wamekataa kuwajibika kuhusu jinai za utawala wao wa zama za ukoloni katika eneo hilo la Kenya.

Waliowasilisha kesi hiyo wanataka serikali ya Uingereza iwaombe radhi na iwarejeshe ardhi zao za jadi walizoporwa na Wazungu.

Kericho ni kati ya maeneo yenye rotuba zaidi nchini Kenya na ni maarufu kwa zao la chai. Idadi kubwa ya watu wa jamii za  Kipsigis na Talai  wanasema walilazimika kuwa maskwota katika zama za ukoloni baada ya ardhi zao za jadi kuporwa.

Mwaka 2013, Serikali ya Uingereza ililazimika kuomba radhi na kukubali kuwalipa fidia maelfu ya wapiganaji wa vita vya uhuru wa Kenya vilivyojulikana kama Mau Mau, kutokana na kuteswa na kutendewa maovu katika miaka ya 1950. Hatua hiyo ilifungua mlango kwa mashtaka mengine dhidi ya Uingereza kutokana na jinai zake katika makoloni yake ya zamani. Tume ya Haki za binadamu ya Kenya inakadiria kwamba Wakenya 90,000 waliuliwa au kukatwa viungo vyao na karibu 160,000 kufungwa, na wengine wengi kuteswa na kubakwa katika zama za ukoloni wa Uingereza.