Apr 24, 2016 14:48 UTC
  • Wanajeshi wa serikali wauawa kaskazini mwa Mali

Duru za usalama nchini Mali zimesema kuwa, watu wenye silaha wamewavamia wanajeshi wa serikali kaskazini mwa nchi hiyo na kuua wanajeshi wawili.

Gazeti la Le Figaro la nchini Ufaransa limezinukuu duru za usalama za Mali zikitangaza leo Jumapili kuwa, jana usiku watu wasiojulikana wenye silaha waliushambulia msafara wa kijeshi katika eneo la Timbuktu, kaskazini mwa Mali na kuua wanajeshi wawili na kumjeruhi mwengine mmoja.

Hata hivyo duru hizo za usalama za Mali hazikutaja wasifu wa wanajeshi hao.

Eneo pana la kaskazini mwa Mali lilianza kushuhudia mashambulizi ya waasi wa Tuareg kabla ya kujitokeza makundi ya kigaidi yenye mfungamano na mtandao wa al Qaida na kulidhibiti eneo hilo.

Maeneo mengi ya kaskazini mwa Mali yanaendelea kudhibitiwa na makundi yenye silaha.

Tangu mwaka 2012, Ufaransa imetuma wanajeshi wake kaskazini mwa Mali kwa madai ya kupambana na makundi yenye misimamo mikali. Hata hivyo kitendo hicho cha Ufaransa kimeongeza machafuko katika eneo hilo badala ya kuyapunguza.

Pamoja na kuweko makubaliano ya amani baina ya serikali na waasi wa Mali, lakini hadi hivi sasa makundi yenye misimamo mikali yana nguvu kaskazini mwa nchi hiyo.

Tags