Rais Kenyatta afuta ajenda ya ubaradhuli katika Kongamano la Kimataifa Nairobi
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amefutilia mbali mpango wowote wa kujumuishwa kadhia ya ubaradhuli kama moja ya ajenda za Kongamano la Kimataifa la Idadi ya Watu litakalofanyika wiki ijayo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi.
Rais Kenyatta amesema, Kenya iko tayari kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa kuhusu idadi ya watu lakini haitaruhusu vitendo ambavyo vinakiuka utamaduni wa Kiafrika.
Ameongeza kuwa, "Tutawakaribisha wageni Nairobi, na tutashiriki kongamano hilo na kusikiliza yatakayojadiliwa, lakini tutasimama imara kupinga kile ambacho hatukubaliani nacho."
Mara kwa mara, Rais Kenyatta amekuwa akishikilia msimamo huo wa kupinga uozo huo, na jitihada za kujumuishwa uhusiano wa aina hiyo katika katiba ya Kenya. Mei 24 mwaka huu, Mahakama Kuu ya Kenya ilifutilia mbali mpango wa kufuta au kuangalia upya sheria zinazoharamisha ubaradhuli nchini Kenya.
Haya yanajiri wakati huu ambapo Uganda inajiandaa kurejesha muswada bungeni ambao utatoa adhabu kali kwa mabaradhuli na wanaoendesha vitendo vichafu vya mahusiano ya watu wa jinsia moja, ikisisitiza kuwa vitendo hivyo vichafu vimeenea sana nchini humo na inabidi sheria kali ziwekwe ili kuvidhibiti.
Aghalabu ya nchi za Afrika zimeharamisha na kupiga marufuku vitendo vya usenge na usagaji, na wanaopatikana na hatia ya kujihusisha na ufuska huo huandamwa na adhabu kali.