Burundi: Waasi wa Rwanda ndio wamewaua askari wetu 8 na kuwajeruhi wengine
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57370-burundi_waasi_wa_rwanda_ndio_wamewaua_askari_wetu_8_na_kuwajeruhi_wengine
Wizara ya Ulinzi pamoja na duru za kijeshi za Burundi zimetangaza kwamba askari wanane wa nchi hiyo wameuawa katika shambulio lililotokea karibu na mpaka wa Rwanda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2019 12:56 UTC
  • Burundi: Waasi wa Rwanda ndio wamewaua askari wetu 8 na kuwajeruhi wengine

Wizara ya Ulinzi pamoja na duru za kijeshi za Burundi zimetangaza kwamba askari wanane wa nchi hiyo wameuawa katika shambulio lililotokea karibu na mpaka wa Rwanda.

Taarifa iliyotolewa leo na Wizara ya Ulinzi na duru za kijeshi za Burundi imesema kuwa makumi ya askari wengine wa nchi hiyo pia hawajulikani walipo baada ya kujiri shambulizi hilo lililoilenga kambi ya askari hao. Aidha imeongeza kwamba hilo ni shambulizi kubwa kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka kadhaa. Emmanuel Gahungano, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Burundi amesema kuwa, kundi moja la wabeba silaha kutoka Rwanda ndilo lililotekeleza shambulizi hilo katika eneo la Twinyoni la mkoa wa Cibitoke na kwamba baada ya hujuma hiyo walikimbilia tena ardhi ya Rwanda.

Askari wa Burundi

Hata hivyo Gahungano hakueleza upana wa hasara ya shambulizi hilo. Burundi ilitumbukia katika machafuko tangu mwaka 2015 baada ya vyama vya upinzani na asasi mbalimbali kupinga uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo wa kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi uliopita. Wapinzani wanadai kuwa hatua ya rais huyo inakinzana na katiba ya Burundi, huku kwa upande wake serikali ikisisitiza kuwa bado haijakiuka katiba. Katika upande mwingine, nchi hiyo na kwa mara kadhaa imekuwa ikiinyoshea kidole cha lawama serikali ya Rwanda kwamba inayaunga mkono makundi ya wabeba silaha yanayoipinga serikali ya Bujumbura, madai ambayo yamekuwa yakikanushwa na serikali ya Kigali.