Watu 24 wapoteza maisha katika maporomoko ya ardhi Kenya
Watu wasiopungua 24 wamepoteza maisha magharibi mwa Kenya kufuatia maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya West Pokot.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Kaunti ya West Pokot, Apollo Okello, tayari wameshapata miili ya watu 12 wakiwemo watoto saba baada ya maporomoko makubwa ya ardhi kukumba vijiji vya Nyarkuliana na Parua Ijumaa usiku kufuatia mvua kubwa ambazo zilinyesha kwa masaa kadhaa. Amesema kunaendelezwa oparesheni za kutafuta miili ya waathirika wa tukio hilo. Mvua hizo aidha zimesebabisha kufungwa sehemu moja ya barabara ya Kitale-Lodwar karibu na Ortum na hivyo kuathiri vibaya shughuli za uokoaji.
Aidha Daraja la Muruny katika eneo hilo limesombwa na mafuriko kufuatia mvua hizo.
Mvua kubwa zimekuwa zikinyesha kote Kenya katika wiki za hivi karibuni na kusababisha hasara kubwa.
Mwezi Aprili mwaka 2018, watu 100 walipoteza maisha kufuatia maporomoko ya ardhi katika maeneo kadhaa ya Kenya huku maelfu wakipoteza makao.