Kiongozi Muadhamu awaasa Wakristo washikamane na mema
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewanasihi wafuasi wa dini ya Kikristo wafungamane na vitendo vyema kama walivyoelekezwa na Nabii Issa Masih (AS).
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika ujumbe wake aliotuma kwa mnasaba wa kumbukumbu ya mazazi ya Nabii Issa (AS), yanayoadhimishwa hii leo na Wakristo kote duniani.
Katika ujumbe huo aliotuma kwenye ukurasa wake wa Twitter, Kiongozi Muadhamu ameandika: Miongozo ya Nabii Issa Bin Maryam (AS), ni miongozo ya kuabudiwa Mungu mmoja, na kupambana na Mafarao na madhalimu.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa, "Kumfuata #YesuKristo kuna maana ya kufungamana na vitendo vyema na kujiweka mbali na nguvu za upotofu, na inatarajiwa kuwa, Waislamu na Wakristo katika kona zote za dunia watashikamana na mafunzo hayo makubwa ya Nabii Issa (AS) katika maisha na matendo yao."
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif ametuma salamu za baraka na pongezi kwa mawaziri wenzake Wakristo kote duniani kwa mnasaba wa kukumbuka mazazi ya Nabii Issa (AS).
Siku kama ya leo miaka 2020 iliyopita, Nabii Issa Masih (AS) alizaliwa katika mji wa Bait Laham (Bethlehem) huko Palestina. Inafaa kuashiria hapa kwamba, tarehe 25 Disemba kila mwaka inajulikana kote duniani hasa kwa Wakristo kuwa ni Sikukuu ya Krismasi.