Tahadhari yatolewa kuhusu hali mbaya ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky
Ofisi ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) kwa mara nyingine tena imeeleza wasiwasi wake kuhusiana na hali mbaya ya kiafya ya kiongozi wake, Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa katia jela ya nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya IMN kupitia mtandao wa Twitter imesema kuwa: Siku 21 zimepita sasa tangu Sheikh Zakzaky na mke wake, Malama Zeenat wahamishiwe katika jela ya serikali ya Nigeria; hali zao za kiafya zinaendelea kuwa mbaya na wanazuiwa kupata huduma na mahitaji ya kimsingi kama dawa na matibabu.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu (Islamic Human Rights Commission (IHRC)) yenye makao yake London nchini Uingereza, Massoud Shajareh amezungumzia hali mbaya ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe na kusema: "Uwezekano wa kuachiwa huru mwanazuoni huyo ni mdogo sana hasa kwa kutilia maanani mashinikizo makubwa yanayofanywa na utawala wa Nigeria dhidi ya Sheikh Zakzaky."
Massoud Shajareh ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kiafya ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na kusema: Mienendo ya utawala wa Nigeria kwa Sheikh Zakzaky na mkewe haviakisi hamu ya utawala huo ya kumuachia huru. Amesema Sheikh Zakzaky anashikiliwa katika jela kuu ya jimbo la Kaduna isiyokuwa na vigezo vya usalama wa kiafya kwa wafungwa wake na ambayo ni miongoni mwa jela hatari sana barani Afrika.
Sheikh Ibrahim Zakzaky, (66) na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Husaynia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.