Mfuasi wa Sheikh Zakzaky auawa na polisi katika maandamano Abuja
Vikosi vya usalama nchini Nigeria vimemuua kwa kumpiga risasi mfuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria katika maandamano ya kulalamikia kuendelea kushikiliwa gerezani kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Duru za habari zinaarifu kuwa, katika maandamano hayo ya jana Jumanne mjini Abuja, maafisa wa polisi walitumia risasi hai na mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo amenukuliwa na jarida la intaneti la The Cable akisema kuwa, "polisi walifyatua risasi hai hewani wakati wakiwakabili waandamanaji, na hapo ndipo risasi ikampiga kichwa mmoja wa waandamanaji."
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba picha za Sheikh Zakzaky, walisikika wakipiga nara za kuikosoa vikali serikali ya Rais Muhammadu Buhari, kwa kuendelea kumshikilia kinyume cha sheria mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Vyombo vya dola vya Nigeria vinaendelea kumshikilia Sheikh Zakzaky katika hali ambayo, tarehe pili Disemba 2016 Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa hukumu kwamba kutiwa mbaroni Sheikh Zakzaky na mkewe ni kinyume cha sheria na kunakinzana na katiba ya nchi hiyo.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.