Misri yawahukumu watu kadhaa kifungo cha maisha jela kwa kujiunga na Daesh
Mahakama Cairo nchini Misri imewahukumu watu wasiopungua 37 vifungo mbalimbali vya jela kikiwemo kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kujiunga na kuliunga mkono genge la uhalifu lenye mfungamano na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Duru za mahakama zimeripoti kuwa, Mahakama ya Uhalifu ya Cairo imewahukumu watu wanane kifungo cha maisha jela na wengine 29 wamehukumiwa vifungo vya jela vya baina ya mwaka mmoja na 15. Watu hao wamekatiwa hukumu hizo baada ya kupatikana na hatia ya kupanga mashambulizi na kueneza aidiolojia ya kundi la kitakfiri la Daesh katika jela za Misri na kufadhili mitandao yao.
Mahakama ya Uhalifu ya huko Cairo imewafutia hatia washukiwa wengine saba. Washtakiwa hao wanaweza kukata rufaa katika Mahakama Kuu ambayo ni mahakama ya ngazi ya juu ya kiraia ya Misri dhidi ya hukumu hizo walizokatiwa.
Katika miaka kadhaa ya karibuni magaidi wamekuwa wakifanya hujuma na mashambulizi makubwa dhidi ya serikali ya Misri wakitumia vibaya hali ya mgogoro iliyojitokeza nchini humo baada kupinduliwa Mohamed Morsi, Rais wa kwanza wa Misri kuwahi kuchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia. Morsi alipinduliwa katika mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai mwaka 2013 yaliyoongozwa na kiongozi wa sasa wa nchi hiyo, Abdel Fattah al Sisi.