UN: Watoto ndio wahanga wakuu wa mapigano eneo la Sahel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58798-un_watoto_ndio_wahanga_wakuu_wa_mapigano_eneo_la_sahel
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mamia ya watoto waliuawa mwaka jana katika mapigano na ghasia zinazoendelea kushuhudiwa katika eneo la Sahel la barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 28, 2020 08:18 UTC
  • UN: Watoto ndio wahanga wakuu wa mapigano eneo la Sahel

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mamia ya watoto waliuawa mwaka jana katika mapigano na ghasia zinazoendelea kushuhudiwa katika eneo la Sahel la barani Afrika.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema watoto 277 ama waliuawa au kujeruhiwa kutokana na mateso makali katika kipindi cha miezi tisa ya kwanza ya mwaka jana 2019 nchini Mali pekee.

Ripoti ya UNICEF imesema idadi hiyo ni mara mbili ikilinganishwa na idadi ya watoto waliouawa au kupata ulemavu wa daima katika ghasia hizo katika kipindi hicho mwaka 2018, na kwamba watoto wadogo wanaendelea kuwa wahanga wakuu wa makabiliano baina ya maafisa usalama na makundi ya kigaidi katika eneo hilo.

Msemaji wa UNICEF amesema ingawaje hawana takwimu rasmi, lakini watoto wengi waliuawa, kuteswa na kubakwa mwaka jana katika nchi za Burkina Faso na Niger. Ripoti hiyo mpya ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa imesema watoto milioni 4.9 katika nchi za eneo la Sahel wanahitaji msaada wa dharura. 

Mgogoro wa chakula katika eneo la Sahel

Msemaji wa UNICEF katika eneo la katikati na magharibi mwa Afrika, Marie-Pierre Poirier amesema mapigano na vita vinavyoshuhudiwa katika eneo hilo la Saleh vimewafanya mamilioni ya watoto wakose mahitaji ya msingi kama chakula, maji, dawa na elimu.

Kwa mujibu wa takwimu za UN, watoto 709,000 wenye chini ya umri wa miaka mitano wanakabiliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu katika nchi za Mali, Burkina Faso na Niger, na kwamba wengine milioni 4.8 wanakodolewa macho na uhaba wa chakula.