Magaidi 120 wauawa kusini magharibi mwa Niger
Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza habari ya kuuawa magaidi 120 na kutekwa magari na vifaa vyao vya kutengenezea mabomu katika operesheni maalumu iliyofanywa na wanajeshi wa nchi hiyo katika eneo la kusini magharibi mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema, tarehe 20 Februari (siku ya Ijumaa) magaidi 120 waliangamizwa katika operesheni kubwa iliyofanyika kwenye eneo la Tillaberi lililoko karibu na mpaka wa Mali na Burkina Faso. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanajeshi wa Ufaransa wameshiriki kwenye operesheni hiyo na hakuna hasara yoyote iliyopatikana upande wa wanajeshi wa serikali na wale wa Ufaransa.
Taarifa hiyo aidha imemnukuu Waziri wa Ulinzi wa Niger, Issouffou Katambe akiwapongeza wanajeshi wa nchi hiyo kwa kuwa na ushirikiano mzuri katika vita dhidi ya ugaidi.
Maafisa wa eneo la Tillaberi wamechukua hatua mbalimbali za kiusalama kama vile kufunga masoko na kupiga marufuku pikipiki katika eneo hilo baada ya magenge ya wakufurishaji kuua wanajeshi 174 wa Niger katika kipindi cha baina ya Disemba 2019 na Januari 2020.
Hali ya hatari imetangazwa kwenye eneo hilo na inaendelea kwa miaka miwili sasa.
Tangu mwaka 2015, Niger imekumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya magenge ya ukufurishaji hasa katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na nchi za Burkina Faso na Mali. Maeneo yaliyoshuhudia zaidi vitendo hivyo vya kigaidi ni ya Tillaberi na Tahoua ambako yamepelekea karibu watu 78,000 kukimbia makazi yao.
Mwaka huu dola la kikoloni la Ufaransa limetangaza kuimarisha wanajeshi wake Afrika Magharibi kwa kuongeza wanajeshi wapya 600 juu ya wanajeshi wake 4,500 walioko kwenye eneo hilo.