Wapinzani 37 wa serikali ya Cairo wahukumiwa kifo nchini Misri
Mahakama ya Misri imewahukumu kifo wanaharakati 37 kwa kile kilichotajwa kuwa ni kuhusika na harakati za makundi ya kigaidi.
Mahakama ya Jinai ya Cairo jana Jumatatu ilimhukumu kifo afisa wa zamani wa jeshi la nchi hiyo, Hisham Ashmawy na watu wengine 36 kwa makosa ya ugaidi. Watu hao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji ya maafisa wa wa polisi, kumuua mwendesha mashtaka mkuu wa zamani Hisham Barakat na vilevile kuhusika na njama ya kutaka kumuua waziri wa zamani wa mambo ya ndani Mohamed Ibrahim. Vilevile wametuhumiwa kuwa walihusika na mashambulizi dhidi ya vituo kadhaa vya usalama nchini Misri.
Hisham Ashmawy ambaye alikuwa afisa wa operesheni maalumu katika jeshi la Misri alifukuzwa rasmi jeshini mwaka 2011 kwa tuhuma kwamba alikuwa akieneza fikra na misimamo mikali na kuchochea machafuko.
Ashmawy alikimbilia nchi jirani ya Libya mwaka 2014 ambako amekuwa akiongoza mashambulizi dhidi ya serikali ya Cairo na mwaka 2018 alikamatwa na wapiganaji wa jenerali muasi, Khalifa Haftari na kurejeshwa nchini Misri.
Watuhumwia wengine 61 wanaotajwa kuwa ni wanachama wa kundi la Ansar Beit Al Maqdis, wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na wengine 85 wamehukumiwa vifungo vya baina ya miaka 5 hadi 15.