Magaidi 50 wa kundi la Boko Haram wauawa huko Niger
Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza kuwa magaidi hamsini wanachama wa kundi la Boko Haram wameangamizwa huko kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema kuwa, magaidi hao waliuawa katika mapigano makali yaliyotokea baina ya pande mbili wakati askari usalama wa nchi hiyo walipozima shambulizi lililofanywa na wapiganaji wa Boko Haram dhidi ya kituo cha utafiti cha jeshi katika eneo la Toumour katika mkoa wa Diffa. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, magaidi hao walishambulia kituo hicho kwa kutumia magari 20 yaliyokuwa yamesheheni silaha.
Ripoti za awali zinasema kuwa, askari mmoja wa serikali ya Niger amejeruhiwa na wapiganaji 50 wa kundi la Boko Haram wameangamizwa.
Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema kuwa jeshi la nchi hiyo liliwafuatilia magaidi waliobakia hadi katika maficho yao kandokando ya Ziwa Chad na kuwatia nguvuni baadhi yao. Jeshi la Niger pia limefanikiwa kuchukua ngawira magari mawili na silaha kadhaa za magaidi hao.
Mwaka 2015 magaidi hao wa Boko Haram pia walishambulia eneo hilo la Toumour.
Magaidi wa kundi la Boko Haram hadi sasa wameua watu wasiopungua elfu 20 katika nchi za Nigeria, Cameroon, Chad na Niger tangu walipoanza hujuma dhidi ya vituo vya serikali, misikiti na makanisa katika eneo la magharibi mwa Afrika mwaka 2009. Zaidi ya raia milioni mbili pia wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na hujuma na mashambulizi ya kundi hilo.