Makumi ya wanakijiji wauawa na magaidi kaskazini mwa Msumbiji
Jeshi la Polisi la Msumbiji limetangaza habari ya kuuawa makumi ya watu katika shambulizi jipya la kigaidi lililotokea huko kaskazini mwa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Msemaji wa polisi ya Msumbiji, Orlando Modumane alisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, wanakijiji 52 waliuawa na wanachama wa genge la kigaidi baada ya kukataa kusajiliwa kujiunga na kundi hilo.
Amesema mauaji hayo yalifanyika Aprili 7 katika kijiji cha Xitaxi wilayani Muidumbe, katika mkoa ambao unaendelea kushuhudia harakati za kigaidi kwa muda sasa wa Cabo Delgado, kaskazini mwa nchi.
Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017 vimekuwa vikishuhudia mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.

Genge hilo la kitakfiri limekuwa likifanya mashambulizi hayo licha ya serikali ya Msumbiji kutuma wanajeshi na polisi katika maeneo hayo ambayo yapo katika mpaka wa nchi hiyo na Tanzania.
Tayari mamia ya washukiwa wa ugaidi wakiwemo raia wa Tanzania wamekamatwa na kupandishwa kizimbani.