Viongozi wa Afrika wakutana Kenya kujadili ujangili na magendo ya vipusa
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ni mwenyeji wa kongamano la viongozi wa bara hilo linalojadili athari za ujangili na magendo ya pembe za ndovu na vifaru, vinavyotishia sekta ya utalii na kuangamiza turathi za kitaifa barani humo.
Viongozi wanaohudhuria kongamano hilo ni pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Ali Bongo wa Gabon na wajumbe 170 kutoka bara Afrika, Marekani, bara Ulaya, China, Russia na New Zealand. Kongamano hilo linalofanyika katika kaunti ya Laikipia linajadili kuhusu namna nchi za bara hilo zitakomesha ujangili na namna ya kulinda asilimia 50 ya ndovu na vifaru wa bara hilo kufikia mwaka 2020.
Hii ni katika hali ambayo, Rais Kenyatta anatazamiwa kuongoza viongozi hao katika zoezi la kuchoma moto zaidi ya tani 100 za pembe za ndovu na vifaru katika makao makuu ya Shirika la Wanyamapori KWS viungani mwa mji mkuu Nairobi.
Mwezi Februari mwaka jana, rais huyo aliteketeza moto tani 15 za pembe za ndovu kwa juhudi za kutokomeza ujangili na biashara haramu ya pembe za wanyamapori hao ambao wako katika hatari ya kutokomea.
Bara la Afrika lilikuwa na ndovu milioni 13 mwaka 1979, lakini kushadidi magendo ya vipusa kumesababisha idadi hiyo kupungua hadi laki 4 hivi.