May 01, 2016 07:38 UTC
  • Nigeria yasisitiza kutekeleza operesheni imara za kijasusi dhidi ya Boko Haram

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Nigeria amesisitiza juu ya udharura wa kutekeleza operesheni imara za kijasusi dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Geoffrey Onyeama ameashiria kushika kasi operesheni za milipuko ya mabomu zinazotekelezwa na wanachama wa kundi la kitakfiri la Boko Haram nchini humo na kubainisha kwamba, kile ambacho leo kinahitajika kwa ajili ya kulisambaratisha kikamilifu kundi la Boko Haram ni kutekelezwa oeresheni za kijasusi dhidi ya wanamgambo hao.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Nigeria amesema kuwa, kundi la wanamgambo wa Boko Haram limepanua wigo wa harakati zake za kigaidi katika nchi za Benin, Cameroon, Chad na Niger hivyo kuna udharura wa kuongezwa zaidi operesheni za kijasusi dhidi ya wanamgambo hao na hivyo kuandaa mikakati imara ya kukabiliana nao.

Hivi karibuni Mkuu wa vikosi vya Kiafrika vya kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram amezitaka nchi zinazoshiriki katika operesheni ya kijeshi dhidi ya wanamgambo hao kufungamana na ahadi zao.

Kundi la Boko Haram lililoanzisha machafuko ya ndani nchini Nigeria mwaka 2009 limeua zaidi ya watu elfu 20 na kulazimisha mamilioni ya wengine kukimbia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.

Tags