Juhudi za Uturuki za kuweko kijeshi katika nchi ya Libya
Baada ya Uturuki kuwa na uingiliaji wa kijeshi katika masuala ya ndani ya Libya na kushiriki pakubwa katika vita vya niaba, sasa viongozi wa Ankara wanazungumzi suala la kuanzisha vituo viwili vya kijeshi katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Kuhusiana na jambo hilo, maafisa wa ngazi za juu katika jeshi la Uturuki wametangaza kuwa, ili kupeleka ndege zisizo na rubani pamoja na zana zingine za kijeshi za anga nchini Libya, kuna udharura wa kuanzishwa vituo na kambi za kijeshi katika nchi hiyo ya Kiafrika.
Endapo Uturuki itafanikiwa kuweko kijeshi nchini Libya, hapana shaka kuwa, ngome za nchi hiyo katika eneo la kaskazini mwa Afrika zitaimarika na kupata nguvu zaidi. Kwa kuzingatia hali ya sasa inayokabiliwa nayo nchi ya Libya hususan kugawanyika nchi hiyo katika sehemu mbili na kuweko serikali mbili mashariki na magharibi mwa nchi hiyo na wakati huo huo kushadidi vita vya niaba nchini humo, ni jambo lisilo mbali kuwa, kuweko kijeshi Uturuki katika nchi hiyo kutashadidisha vita vya niaba na kuvuruga zaidi hali ya mambo nchini humo.
Katika hali ambayo, katika zama hizi serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan imeamua kuweka katika sera zake siasa zenye muelekeo wa utawala wa Othmania, makubaliano ya mwaka mmoja uliopita kati ya nchi hiyo na Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya yataisaidia Ankara katika kusukumu mbele gurudumu la malengo yake yaliyoainishwa hapo kabla. Katika zama za utawala wa Othmania (Ottoman Empire), Libya ilikuwa moja ya maeneo yaliyoyokuwa yakipendwa na watawala wa wakati huo. Katika zama hizi na katika miaka ya huko nyuma pia, Uturuki ilikuwa na uhusiano mzuri na Libya chini ya uongozi wa kanali Muammar Gaddafi.
Sehemu ya uhusiano huo ilikuwa katika masuala ya kiuchumi, kuweko wawekezaji wa Kituruki nchini Libya ambapo uhusiano wa kiuchumi na nchi hiyo ya Kiafrika ulihesabiwa kuwa upande muhimu wa ushirikiano baina ya pande mbili hizo.
Kwa maneno mengine ni kuwa, moja ya nchi zilizodhurika kiuchumi kutokana na kuangushwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi nchini Libya ilikuwa ni Uturuki. Pamoja na hayo, viongozi wa Ankara waliendelea kufuatilia kwa karibu matukio ya nchi hiyo na hivi sasa baada ya kupita miaka kadhaa tangu kuondolewa madarakani Gaddafi, viongozi wa Uturuki kwa mara nyingine tena wameibuka na kuwa waungaji mkono wa moja ya serikali za sasa nchini Libya.
Ni jambo lililo wazi kwamba, eneo la kaskazini mwa Afrika lina umuhimu mkubwa kwa Uturuki. Baada ya siasa za Uturuki huko nchini Misri na himaya yake kwa serikali ya Ikhwan al-Muslimin kwa namna fulani kukabiliwa na mkwamo baada ya Jenerali Abdul-Fatah al-Sisi kumpindua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Muhammad Mursi, watawala wa Ankara hawakukata tamaa bali wameendelea na mipango yao huko kaskazini mwa Afrika. Sambamba na kuongezeka maslahi ya kiuchumi ya Uturuki na kuwa na utegemezi mkubwa nchi hiyo wa kudhamini nishati kutoka nje ya nchi na wakati huo huo kuweko juhudi za kudhamini usalama wa nishati kwa kupata vyanzo vipya vya nishati mashariki mwa Mediterania sanjari na kustafidi na vyanzo vya uchumi vilivyopo katika nchi hiyo, inaonekana kuwa, viongozi wa Ankara wana mipango ya kuhakikisha wanakuweko katika Bahari ya Mediterania.
Hapana shaka kuwa, makubaliano ya Uturuki na serikali ya Fayez al-Sarraj, Kiongozi wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya ambayo inakubaliwa na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa na akthari ya mataifa ya dunia, yamesaidia kufikiwa malengo kama haya ya kuweko kijeshi katika Bahari ya Mediterania.
Libya inahesabiwa kuwa, moja ya nchi muhimu za Kiafrika pambizoni mwa Bahari ya Mediterania kwa Uturuki kutokana na kuwa na sifa maalumu. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana Uturuki inafanya juhudi kuhakikisha kuwa, Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inakuwa na uthabiti katika maeneo yote ya nchi hiyo na katika uwanja huo, imesimama kukabiliana na jenerali Khalifa Haftar na hata waungaji mkono wake katika eneo kama Misri, Ugiriki na Imarati.
Hata hivyo swali la kujiuliza ni je siasa hizo za Uturuki hatimaye zitafikia tamati kwa maslahi ya Ankara? Ukweli wa mambo ni kuwa, kuwepo kwa kaumu mbalimbali kunaweza kuwa kizingiti kikuu kwa Uturuki kwa ajili ya kuweko kwa muda mrefu katika nchi ya Libya.