Maelfu waandamana Mali wakitaka rais wa nchi hiyo aachie ngazi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61711-maelfu_waandamana_mali_wakitaka_rais_wa_nchi_hiyo_aachie_ngazi
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Mali wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu Bamako, wakishinikiza kujiuzulu Rais Ibrahim Boubacar Keita wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 20, 2020 02:10 UTC
  • Maelfu waandamana Mali wakitaka rais wa nchi hiyo aachie ngazi

Makumi ya maelfu ya wananchi wa Mali wamefanya maandamano makubwa katika mji mkuu Bamako, wakishinikiza kujiuzulu Rais Ibrahim Boubacar Keita wa nchi hiyo.

Waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara za kulaani uongozi mbaya na kashfa za ufisadi zinaoikabili serikali ya Rais Keita.

Katika maandamano hayo ya jana Ijumaa, Cheick Oumar Sissoko, kiongozi wa upinzani nchini humo amewaambia wafuasi wake walioshiriki maandamano hayo kuwa, "tumeafikiana kuunganisha nguvu na kambi zetu zote hadi pale rais atakapojiuzulu."

Keita ambaye alichaguliwa kuwa rais wa Mali kwa muhula wa pili mwaka 2018, anaandamwa na ukosoaji mkubwa kwa kushindwa kuimarisha usalama eneo la kaskazini mwa nchi, kufeli kuipatia ufumbuzi migomo ya walimu, kushindwa kulishughulikia janga la corona na mvutano wa kisiasa uliosababaishwa na uchaguzi tata wa bunge wa mwezi Machi mwaka huu.

Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali anayeandamwa na mashinikizo ya kujiuzulu

Itakumbukwa kuwa, Mali imekuwa katika mivutano ya kisiasa tangu kuibuka machafuko nchini humo mwaka 2012 yaliyosababisha uasi wa baadhi ya wanajeshi na kumpindua Rais Amadou Toumani Toure ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa muda kwa miaka 10.

Hali hiyo ya mivutano ya kisiasa ilitoa mwanya kwa Ufaransa kuingilia kati kijeshi nchini humo na kuiondoa madarakani serikali hiyo ya kijeshi mwaka 2013.