Jeshi la Rwanda laua watu 4 waliobeba silaha kutoka Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i61874-jeshi_la_rwanda_laua_watu_4_waliobeba_silaha_kutoka_burundi
Jeshi la Rwanda limetangaza habari ya kuua watu wanne waliokuwa wamebeba silaha raia wa Burundi kusini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 28, 2020 03:10 UTC
  • Jeshi la Rwanda laua watu 4 waliobeba silaha kutoka Burundi

Jeshi la Rwanda limetangaza habari ya kuua watu wanne waliokuwa wamebeba silaha raia wa Burundi kusini mwa nchi hiyo.

Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Rwanda imesema: Wabeba silaha karibu 100 wasiojulikana jana walivamia kituo cha kiulinzi cha Ruheru yapata kilomita moja mpakani na Burundi, kwa lengo la kuwadhuru wakazi wa kijiji hicho kilichoko katika mkoa wa Cibitoke. Wavamizi wanne wameuawa katika makabiliano hayo yaliyodumu kwa dakika 20 hadi 30 hivi, kabla ya wengine kukimbia na kurundi nchini Burundi.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanajeshi watatu wa Rwanda wamepata majeraha madogo katika makabiliano hayo, na kwamba wabeba silaha watatu kutoka Burundi wametiwa mbaroni. Jeshi la Ulinzi la Rwanda limesema linafuatilia kupitia njia za kidiplomasia hujuma hiyo, ambayo ni katika wimbi la mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na wavamizi kutoka Burundi.

Burundi na Rwanda zimekuwa katika mzozo tangu kulipojiri jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya aliyekuwa rais wa Burundi, hayati Pierre Nkurunziza mwezi Mei mwaka 2015.

Ramani inayoonyesha mpaka wa Rwanda na Burundi

Novemba mwaka jana, Wizara ya Ulinzi pamoja na duru za kijeshi za Burundi zilitangaza kwamba askari wanane wa nchi hiyo wameuawa katika shambulio lililotokea karibu na mpaka wa Rwanda.

Burundi imekuwa ikiinyoshea kidole cha lawama serikali ya Rwanda kwamba inayaunga mkono makundi ya wabeba silaha yanayoipinga serikali ya Bujumbura, madai ambayo yamekuwa yakikanushwa na serikali ya Kigali.