HRW: Makaburi ya umati yagunduliwa kaskazini mwa Burkina Faso
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetangaza habari ya kugunduliwa makaburi ya umati yenye maiti 180 katika mji wa Djibo, kaskazini mwa Burkina Faso.
Shirika hilo linawatuhumu maafisa usalama wa Burkina Faso kuwa wamehusika na mauaji hayo ya makumi ya watu waliowakamata katika operesheni zao dhidi ya makundi ya kigaidi.
Hata hivyo, Moumina Cheriff Sy, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo amesema serikali itachunguza jinai hiyo na kueleza kwamba yumkini mauaji hayo yalifanywa na wanachama wa magenge ya kigaidi waliovalia magwanda ya kijeshi waliyoyaiba.
Ripoti ya HRW imesema mauaji hayo ya raia yalifanyika baina ya Novemba mwaka jana 2019 na Juni mwaka huu katika mji wa Djibo, kaskazini mwa nchi, wakati wa operesheni za maafisa usalama za kupambana na ugaidi.
Aprili mwaka huu, Corinne Dufka, Mkurugenzi wa Human Rights Watch katika eneo la Sahel, Afrika Magharibi alisema katika ripoti kuwa, "kitendo cha maafisa usalama kuua watu ambao hawajajizatiti kwa silaha ni cha fedheha na kinachotia doa operesheni za kupambana na magenge ya kigaidi."
Alisema maafisa usalama wa Burkina Faso wameua raia 30 wasio na hatia katika operesheni zao dhidi ya makundi ya kigaidi na kuitaka serikali ya Ougadougou kuchunguza mauaji hayo na kuwafikisha mbele ya sheria waliotenda jinai hiyo, kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mbali na mamia kuuawa, zaidi ya watu elfu nne wanalazimika kuhama nyumba zao karibu kila siku nchini Burkina Faso kutokana na kuongezeka kiwango na idadi ya mashambulio yanayofanywa na makundi yanayobeba silaha dhidi ya raia wa nchi hiyo.