Watu 15 wauawa katika shambulizi la wabeba silaha Burundi
(last modified Tue, 25 Aug 2020 03:38:39 GMT )
Aug 25, 2020 03:38 UTC
  • Watu 15 wauawa katika shambulizi la wabeba silaha Burundi

Kwa akali watu 15 wameuawa baada ya watu waliojizatiti kwa silaha kushambulia wakazi wa eneo moja huko kusini mwa Burundi.

Haijabainika iwapo waliouawa katika shambulizi hilo ni wakazi wa eneo lililoshambuliwa, waasi walioshambulia au maafisa usalama.

Duru za habari zinaarifu kuwa, wilaya ya Bugarama iliyoko katika mkoa wa Rumonge kusini mwa Burundi inashuhudia mapigano makali tokea Jumapili, na vita hivyo viliendelea hadi jana Jumatatu. 

Mmoja wa mashuhuda wa shambulizi hilo amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, "watu waliobeba bunduki waliwateka wakazi waliokutana nao na kisha kuwaua kabla ya kujiri makabiliano makali baina yao na askari jeshi."

Wakimbizi Burundi

Afisa mmoja wa serikali ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema mashambulizi ya namna hii yalitazamiwa kuanzishwa na waasi wanaopinga mpango wa serikali wa kuanza kuwarejesha nchini wakimbizi raia wa nchi hiyo walioko Rwanda. 

Rwanda ni mwenyeji wa maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi, waliokimbia vita na mapigano nchini kwao tokea mwaka 2015.