Kundi la kwanza la wakimbizi wa Burundi larejea nyumbani kutoka Rwanda
Mamia ya wakimbizi raia wa Burundi walioko nchini Rwanda wameanza kurejea nchini kwao, miaka mitano baada ya kukimbia mapigano na ghasia za kisiasa.
Wakimbizi karibu mia tano wa Burundi walirejea nchini kwao jana Alkhamisi, hili lilikiwa ni kundi la kwanza la wakimbizi Warundi kurejea nchini, tokea nchi hiyo ishuhudie machafuko ya kisiasa yaliyosababishwa na hatua ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza, kugombea muhula wa tatu kinyume na katiba ya nchi.
Warundi hao wamenukuliwa na vyombo vya habari wakisema kuwa, wameamua kurejea nyumbani wakiwa na imani ya kutengeneza mustakabali wao na wa taifa lao, kwa kuwa nchi hiyo hivi sasa ina kiongozi mpya.
Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi alichukua hatamu za uongozi mwezi Juni mwaka huu, kurithi mikoba ya Pierre Nkurunziza.
Kabla ya kuabiri basi la kuwasafirisha kwenda Burundi wakitokea Rwanda, wakimbizi hao wamefanyiwa vipimo vya ugojwa wa Covid-19.
Siku chache nyuma, watu 15 waliuawa baada ya watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha kushambulia wakazi wa eneo moja huko kusini mwa Burundi. Afisa mmoja wa serikali ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema shambulizi hilo lilifanywa na waasi wanaopinga mpango wa serikali wa kuanza kuwarejesha nchini wakimbizi raia wa nchi hiyo walioko Rwanda.
Rwanda ni mwenyeji wa makumi ya maelfu ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi, waliokimbia vita na mapigano nchini kwao tokea mwaka 2015.