Sep 27, 2020 07:59 UTC
  • Waliouawa katika shambulizi la Boko Haram Nigeria waongeza

Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi ya msafara wa Gavana wa jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria imeongezeka na kufikia watu 30.

Duru za kiusalama zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa, miili zaidi ya wahanga wa shambulizi hilo imepatikana. Waliouawa katika shambulizi hilo ni pamoja na maafisa 12 wa polisi, wanajeshi watano, raia 9 na wapiganaji wanne wa kundi linaloungwa mkono na serikali.

Msafara huo wa Gavana wa Borno, Babagana Umara Zulum ulishambuliwa siku ya Ijumaa karibu na mji wa Baga katika fukwe za Ziwa Chad, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, ambapo watu 11 wakiwemo walinzi wa gavana huyo waliripotiwa kuuawa.

Shambulizi hilo lilijiri masaa machache baada ya jeshi la Nigeria kutangaza kuwa limewaua makamanda kadhaa muhimu wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika operesheni kubwa ya jeshi hilo katika jimbo la Borno.

Magaidi wa Boko Haram

Aidha wiki iliyopita pia, jeshi la Nigeria lilitangaza habari ya kuuawa wanachama 16 wa kundi la kigaidi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika hujuma za Boko Haram tokea mwaka 2009 katika nchi nne za magharibi mwa Afrika za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon, na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi hayo.

Tags