Jeshi la Rwanda lakamata wanamgambo 19 wa Burundi mpakani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i63810-jeshi_la_rwanda_lakamata_wanamgambo_19_wa_burundi_mpakani
Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) limewatia mbaroni wanamgambo 19 wa Burundi waliokuwa wamejizatiti kwa silaha katika mpaka wa nchi mbili hizo jirani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 04, 2020 07:35 UTC
  • Jeshi la Rwanda lakamata wanamgambo 19 wa Burundi mpakani

Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) limewatia mbaroni wanamgambo 19 wa Burundi waliokuwa wamejizatiti kwa silaha katika mpaka wa nchi mbili hizo jirani.

Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na RDF inasema, wanamgambo hao wa kundi la 'Red Tabara' ambao waliingia nchini Rwanda kinyume cha sheria, walikamatwa na askari wa RDF katika msitu wa Nyungwe, wilayani Nyaruguru.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, tukio hilo lilifanyika Septemba 29, na kwamba tayari Jeshi la Ulinzi la Rwanda limeitaka jumuiya ya pamoja ya usalama ya kieneo ya EJVM ichunguze tukio hilo.

Burundi na Rwanda zimekuwa katika mzozo tangu kulipojiri jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya aliyekuwa rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza mwezi Mei mwaka 2015. 

Wanajeshi wa Rwanda

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, Jeshi la Rwanda lilitangaza habari ya kuua watu wanne waliokuwa wamebeba silaha raia wa Burundi kusini mwa nchi hiyo, huku wengine wakimbia na kurundi nchini Burundi.

Kadhalika Novemba mwaka jana, Wizara ya Ulinzi pamoja na duru za kijeshi za Burundi zilitangaza kwamba askari wanane wa nchi hiyo wameuawa katika shambulio lililotokea karibu na mpaka wa Rwanda.