Waalgeria wahimizwa kuipigia kura katiba mpya ya nchi hiyo
(last modified Sat, 24 Oct 2020 04:21:06 GMT )
Oct 24, 2020 04:21 UTC
  • Waalgeria wahimizwa kuipigia kura katiba mpya ya nchi hiyo

Wananchi wa Algeria wamehimizwa kuipigia kura ya ndio katiba mpya katika zoezi la kura ya maoni lililopangwa kufanyika Novemba Mosi mwaka huu. Serikali imeitaja kura hiyo ya maoni kuwa msingi wa nchi mpya.

Rais Abdelmadjed Tebboune wa Algeria amesema kuwa katiba mpya italeta uhuru na demokrasia nchini humo. Hata hivyo kumekuwa na maoni tofauti miongoni mwa wananchi na makundi ya Algeria. Harakati ya Maandamano ya Wananchi wa Algeria iliyomng'oa madarakani mtawala wa zamani wa nchi hiyo, Abdelaziz Bouteflika, imetaka kususiwa kura  hiyo ya maoni sambamba na kuukana uongozi wa Rais Tebboune.

Rais aliyeondolewa madarakani wa Algeria Abdelaziz Bouteflika 

Kwa mujibu wa rasimu ya katiba mpya ya Algeria, katiba mpya ya nchi hiyo itampatia Waziri Mkuu na Bunge madaraka zaidi ya kuiongoza nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika iliyo na jamii ya watu milioni 45. 

Inafaa kuashiria hapa kuwa, katiba ya sasa ya Algeria imefanyiwa marekebisho mara kadhaa tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa mkoloni Ufaransa. Katiba hiyo imefanyiwa marekebisho hayo katika kipindi cha miaka 20 ya kuweko madarakani Bouteflika ili kukidhi matakwa yake.

Wakosoaji wengine wa rasimu hiyo ya katiba ya Algeria wanasema imeandaliwa ili kudumisha mfumo wa Rais na jeshi lenye nguvu na mamlaka makubwa zaidi huku ikikandamiza vyombo vya mahakama na Bunge kama taasisi  za uangalizi.  

Tags