Kiongozi wa Upinzani DRC atangaza rasmi kugombea urais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6436-kiongozi_wa_upinzani_drc_atangaza_rasmi_kugombea_urais
Moise Katumbi, kiongozi mashuhuri wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC ametangaza rasmi nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwezi Novemba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2016 03:55 UTC
  • Kiongozi wa Upinzani DRC atangaza rasmi kugombea urais

Moise Katumbi, kiongozi mashuhuri wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC ametangaza rasmi nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwezi Novemba.

Rais wa sasa Joseph Kabila anatakiwa kuachia ngazi wakati huu kwa mujibu wa katiba lakini wapinzani wake wanasema anapanga njama ya kuendelea kubakia madarakani.

Tangazo la Katumbi yamkini likaongeza joto la kisiasa nchini humo ambapo watu zaidi ya 40 wameuawa tokea Januari 2015 katika maandamano ya kupinga mabadiliko ya katiba yenye lengo la kumuwezesha Kabila aendelee kutawala.

Katika ujumbe aliotuma kwa njia ya mtandao wa kijami wa Twitter, Katumbi ametangaza rasmi kukubali kuwania urais. Hivi karibuni muungano wa Upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umemtangaza Moise Katumbi kuwa mgombea wake katika uchaguzi ujao wa rais .

Katumbi alikuwa gavana wa eneo la Katanga kutoka mwaka 2007 hadi Septemba mwaka jana wakati alipojiondoa katika chama cha rais Kabila, akikituhumu kupanga njama ya kumbakisha Kabila madarakani zaidi ya mihula yake miwili ya kikatiba. Kabila aliingia madarakani DRC mwaka 2001.

Hivi karibuni Tume Huru ya Uchaguzi Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) iliomba muda zaidi wa miezi 16 kujitayarisha kwa ajili ya kuandaa zoezi la uchaguzi wa rais.

Vyama vya upinzani vinasisitiza kuwa uchaguzi DRC lazima ufanyike katika kipindi kilichoainishwa.