Nov 10, 2020 07:21 UTC
  • Zaidi ya 50 wauawa kwa kukatwa vichwa na magaidi huko Msumbiji

Makumi ya watu wakiwemo vijana mabarobaro wameuawa kwa kukatwa vichwa na genge la wanamgambo wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS), kaskazini mashariki mwa Msumbiji.

Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa, wanaume zaidi ya 50 wameuawa baada ya magaidi hao kuwashambulia walipokuwa katika sherehe za kuwapasha tohara vijana katika wilaya ya Muidumbe iliyoko katika mkoa wa Cabo Delgado.

Viwiliwili vya waliouawa na vilivyokuwa vimetapakaa hadi umbali wa mita 500 kando kando ya msitu mmoja ulioko wilayani hapo, viliokotwa jana Jumatatu na kukabidhiwa familia kwa ajili ya kuzikwa hii leo.

Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo hao wameshadidisha vitendo vyao vya kikatili kama mauaji, kukata watu vichwa, kuteka nyara na hata kuchoma moto nyumba zilizoko katika mkoa huo wa kaskazini mwa nchi.

Nyumba zilizochomwa moto na magaidi Cabo Delgado

Watu zaidi ya elfu mbili wameuliwa katika vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017, kutokana na mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.

Aidha mapigano hayo kati ya wanamgambo wenye silaha na wenye misimamo ya kuchupa mipaka na vikosi vya serikali ya Msumbiji yamezusha hofu miongoni mwa raia na kuwafanya laki nne miongoni mwao wakimbie makazi yao.

Tags