Serikali ya Uganda yapiga marufuku televisheni kuonesha maandamano ya wapinzani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6490-serikali_ya_uganda_yapiga_marufuku_televisheni_kuonesha_maandamano_ya_wapinzani
Serikali ya Uganda imepiga marufuku kanali za televisheni za nchi hiyo kuonesha moja kwa moja maandamano ya wapinzani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 06, 2016 00:02 UTC
  • Serikali ya Uganda yapiga marufuku televisheni kuonesha maandamano ya wapinzani

Serikali ya Uganda imepiga marufuku kanali za televisheni za nchi hiyo kuonesha moja kwa moja maandamano ya wapinzani.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Waziri wa Habari Jenerali Jim Muhwezi, serikali ya Kampala imesema kuanzia sasa ni marufuku kwa kanali yoyote ya televisheni kuonesha matangazo ya moja kwa moja ya maandamano yatakayoitishwa na kiongozi wa upinzani Dokta Kizza Besigye. Muhwezi ameonya kuwa chombo chochote cha habari kitakachokiuka amri hiyo mpya kinaweza kufutiwa leseni yake.

Dokta Kizza Besigye, aliyegombea urais kwa tiketi ya chama cha FDC pamoja na wagombea wengine wa kiti hicho wamepinga matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyompa ushindi Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi uliofanyika Februari 18 mwaka huu wakisema hakushinda kihalali.

Besigye, ambaye ni mpinzani na hasimu mkuu wa Museveni jana alitoa wito kwa wafuasi wake kufanya maandamano ya kupinga ushindi wa Rais Museveni.

Kwa mujibu wa Waziri wa Habari wa Uganda, lengo la maandamano yanayoitishwa na kiongozi huyo wa upinzani ni kuvuruga sherehe ya kuapishwa Museveni iliyopangwa kufanyika tarehe 12 mwezi huu.

Hii si mara ya kwanza kwa ushindi wa Rais Yoweri Museveni ambaye amechaguliwa kwa mara ya tano kulalamikiwa na wapinzani nchini humo.../