Maalim Seif ateuliwa kuwa makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amemteua mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar.
Kwa mujibu wa katibu mkuu kiongozi wa Zanzibar, Dk Abdulhamid Yahya Mzee, uteuzi huo umeanza jana Jumapili.
Hayo yanajiri wakati ambao, chama cha ACT-Wazalendo kilikataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa kusema kwamba yalikua batili.
Chama hicho sasa kinasema baada ya majadiliano ya muda mrefu pamoja na kupokea maoni ya wanachama wake, kimeamua kuungana na serikali ya chama tawala kwa ajili ya kuendesha nchi.
Dk Abdulhamid Yahya Mzee amesema uteuzi umezingatia matakwa ya kifungu cha 9(3) cha katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinachosomeka kwamba, muundo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia.
Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametuma ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter na kusema anadiriki ghadhabu na ukosoaji uliopo kufuatia uamuzi wa chama chake kuheshimu katiba ya Zanzibar kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Amesema huo haukua uamuzi wanaoupenda lakini ni uamuzi unaohitajika katika kipindi hiki.

Kwa mujibu wa Chama cha ACT Wazalendo, hali ilivyo kwa sasa Zanzibar inahitaji busara kubwa katika kuponya majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo, ili kuhakikisha kuwa matukio ya namna hiyo hayajirudii tena.
Mwezi Oktoba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilimtangaza Dkt Hussein Mwinyi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Rais Mteule wa Zanzibar baada ya kupata ushindi wa kura 380,402 sawa na 76.27%. akifuatiwa na Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 96,103 sawa na asilimia 19.87.
Baada ya kutangazwa mshindi, Mwinyi alisema kuwa Zanzibar mpya itajengwa na Wazanzibari wote bila kujali itikadi zao na kwamba, Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko tofuati za Wazanzibari.