Pezeshkian: Maingiliano makubwa ya kiutamaduni baina ya Iran na Tanzania ni fursa ya kipekee
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa maingiliano makubwa ya kiutamaduni baina ya Iran na baadhi ya maeneo ya Tanzania hasa Zanzibar, ni fursa nzuri ya kustawishwa zaidi na zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili.
Masoud Pezeskhian alisema hayo jana Jumatano wakati alipoonana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliyekuja hapa Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa rais huyo wa 14 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais wa Iran amesema, anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 14 wa Iran na kusisitiza kuwa, Tehran iko tayari kustawisha kwa kiwango kikubwa ushirikiano wake na Tanzania katika nyuga tofauti za kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania kwa mara nyingine amempongeza Daktari Pezeshkian kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa 14 wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kumuombea mafanikio katika kazi zake.
Vile vile Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema, uhusiano wa kihistoria baina ya Iran na Tanzania ni wa maelfu ya miaka na kwamba kuna idadi kubwa ya Washirazi wa Iran waliohamia visiwani Zanzibar miaka mingi nyuma na kueneza utamaduni wa Kiirani na hata lugha ya Kifarsi katika maeneo hayo.
Vilevile amemtaka Rais Pezeshkian aihesabu Tanzania kuwa ni kama nchi yake ya pili na amewakaribisha Wairani kuitembelea Tanzania ili kuziti kutia nguvu ushirikiano wa mataifa haya mawili katika nyuga tofauti hasa upande wa masuala ya kiuchumi na kiutamaduni.