Rais wa Misri atupiwa lawama nyingine
(last modified Tue, 08 Dec 2020 07:28:49 GMT )
Dec 08, 2020 07:28 UTC
  • Rais wa Misri atupiwa lawama nyingine

Mashirika mengi ya haki za binadamu yamemtupia lawama chungu nzima Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri wakati huu wa ziara yake mjini Paris, Ufaransa.

Televisheni ya France 24 imeripoti kuwa, sambamba na ziara ya siku 3 ya Abdel Fattah el Sisi huko Ufaransa, taasisi na mashrika mbalimbali ya haki za binadamu yameporomosha lawama zao kwa rais huyo kutokana na hali mbaya ya haki za binadamu nchini Misri.

Mashirika hayo yameilaumu pia serikali ya Ufaransa kwa kuiuzia Misri marundo ya silaha na vifaa vya kuchunguza raia. 

Antoine Madeleine, mmoja wa viongozi wa Umoja wa Kimataifa wa Haki za Binadamu amelalamikia hali mbaya ya haki za binadamu nchini Misri na kusema kuwa, ripoti zao zinaonesha kwamba vifaa na silaha hizo za Ufaransa zinatumiwa kwa kiwango kikubwa na viongozi wa Misri kukandamiza raia na wapinzani wao.

Serikali ya Misri inatuhumiwa vikali kuvunja haki za binadamu

 

Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri, jana Jumatato alionana na kufanya mazungumzo na rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, mjini Paris.

Mashirika mengi yasiyo ya kiserikali yamelalamikia vikali kitendo cha dola kongwe la kikoloni la Ulaya yaani Ufaransa, cha kuiuzia serikali ya Misri, silaha na vifaa vya kuchunguza raia. Akijibu lawama hizo, Macron amesema katika mazungumzo yake na el Sisi kwamba mauzo ya silaha za Ufaransa kwa Misri hayashurutishwi na kuboreshwa hali ya haki za binadamu nchini humo.

Mashirika ya haki za binadamu yanasema kuwa, sasa hivi wanaharakati 60 elfu wa haki za binadamu na kisiasa wako katika korokoro na jela za serikali ya Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri.

Tags