ICC: Tuna ushahidi wa kutosha wa kuwafungulia mashtaka maafisa wa Nigeria
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC, amesema kuwa, ana ushahidi wa kutosha wa kuweza kuwafungulia mashtaka maafisa wa Nigeria kuhusu mateso na ukandamizaji waliofanyiwa wananchi wa nchi hiyo.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana Ijumaa, Fatoum Bensouda amesema, uchunguzi wa miaka 10 umekusanya ushahidi wa kutosha wa uhalifu dhidi ya binadamu na jinai za kivita zilizofanywa na kundi la Boko Haram na maafisa usalama wa Nigeria.
Hatua inayofuatia sasa ni kupata idhini kutoka kwa majaji wa ICC ya kuweza kufungua mashtaka dhidi ya wahusika wa ukandamizaji na jinai hizo.
Sehemu nyingine ya taarifa ya Bensouda imesema, kama tunavyozingatia kufanya uchunguzi usiopendelea upande wowote, tunatamani pia kupata ushirikiano tunaoutaka kutoka kwa Serikali ya Nigeria ili uadilifu uweze kutendeka.
Amesema, uchunguzi wa awali ulioanza mwaka 2010, umechukua muda mrefu kutokana na vipaumbele vilivyotolewa na ofisi yake vya kupata uungaji mkono wa maafisa wa Nigeria katika uchunguzi wake kuhusu uhalifu na jinai hizo ndani ya maeneo husika.

Genge la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram limekuwa likifanya jinai na mauaji ya raia kwa zaidi ya miaka 10 hivi sasa nchini Nigeria. Maafisa wa kijeshi na vikosi vingine vya usalama vya Nigeria navyo vinalaumiwa kwa kutenda jinai za kivita.
Baada ya taarifa hiyo ya jana ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuunga mkono juhudi za kufanyika uchunguzi kamili kuhusu jinai hizo likisema ni suala ambalo lilikuwa linasubiriwa kwa hamu kwa muda mrefu.