Dec 18, 2020 07:22 UTC
  • Mamia ya wanafunzi waliotekwa na Boko Haram waachiwa huru

Vyombo vya usalama vya Nigeria vimetangaza habari ya kuwanusuru karibu wanafunzi wavulana 350 kati ya 520 wa shule ya upili ya eneo la Kankara kaskazini magharibi mwa nchi, waliokuwa wametekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Gavana wa jimbo la Katsina, Aminu Bello Masari amethibitisha habari hiyo ya kuokolewa wanafunzi hao na kubainisha kuwa, "nadhani tumefanikiwa kunusuru aghalabu ya vijana waliokuwa wametekwa nyara."

Msemaji wa Gavana huyo, Abdul Labaran amesema wanafunzi hao wa kiume kwa sasa wamepelekwa katika makao makuu ya jimbo la Katsina na karibuni watajumuika tena na jamaa zao.

Haya yanajiri masaa machache baada ya genge hilo la ukufurishaji kusambaza mkanda wa video unaowaonyesha makumi ya wanafunzi hao liliowateka nyara wiki iliyopita.

Mwaka 2014 kundi hilo la kigaidi liliwateka nyara pia wanafunzi wa kike 200 huko Chibok, Nigeria 

Msemaji wa Gavana wa Katsina amesema video hiyo iliyosambazwa na Boko Haram katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ni ya kweli, lakini sauti ya mzungumzaji anayedaiwa kuwa kinara wa kundi hilo, Abubakar Shekau ni bandia.

Labaran amesema hakuna mwanafunzi yoyote aliyeuawa katika tukio hilo la utekaji, kauli inayokinzana na ya mwanafunzi mmoja aliyezungumza katika mkanda wa video wa Boko Haram, akidai kuwa baadhi ya wanafunzi wenzake wameuawa katika shambulizi la anga lililofanywa na ndege za kivita za jeshi la Nigeria.

Tags