Dec 30, 2020 14:55 UTC
  • Shambulio la bomu la Boko Haram laua askari 11 Nigeria

Maafisa usalama 11 wakiwemo wanajeshi wanne wameuawa katika shambulio la bomu la kutegwa ardhini la kundi la kigaidi la Boko Haram katika jimbo la Borno huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Duru za habari zinaarifu kuwa, wawindaji saba waliokuwa wakilisaidia jeshi la Nigeria kupambana na Boko Haram wameuawa pia katika shambulio hilo la jana Jumanne.

Habari zinasema kuwa, 11 hao walipoteza maisha baada ya gari lililokuwa limewabeba kukanyaga bomu lililokuwa limetegwa ardhini na magaidi wa Boko Haram katika kijiji cha Kayamla kilichoko mjini Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno.

Jumatatu iliyopita, wanajeshi wanne wa Nigeria walipoteza maisha baada ya gari lao kukanyaga bomu jingine la kutegwa ardhini na wanamgambo hao wakufurishaji katika kijiji cha Logomani, mpakani mwa nchi hiyo na Cameroon.

Ramani inayoonesha mji wa Maiduguri wa kaskazini mashariki mwa Nigeria

Zaidi ya watu elfu 20 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa genge hilo.

Harakati za kundi hilo la kigaidi hivi sasa zimeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad.

Tags