CDC yaonya dhidi ya hatari ya kuicheleweshea Afrika chanjo ya Covid-19
Taasisi kuu ya kudhibiti magonjwa barani Afrika imetahadharisha kuwa, dunia itajiingiza katika matatizo ya kimaadili iwapo nchi za Afrika zitachelewa kupokea chanjo za ugonjwa wa Covid-19, wakati huu ambapo aghalabu ya nchi tajiri duniani zimeanza kuwachanja wananchi wao.
Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) kilitoa indhari hiyo jana Alkhamisi kisisitiza kuwa, inatajiwa kuwa kampeni ya chanjo ya corona barani Afrika inatazamiwa kuanza mwezi Aprili mwaka huu 2021.
John Nkengasong, Mkuu wa Africa CDC amewaambia waandishi wa habari kuwa, "kusubiri hadi wakati huo (mwezi Aprili) ni muda mrefu sana haswa kwa kuzingatia kuwa virusi hivi vinasambaa kwa kasi sana. Wimbi la pili la janga la corona lipo Afrika hivi sasa kwa kasi kubwa."
Kwa mujibu wa takwimu za CDC, bara la Afrika limeshuhudia ongezeko la asilimia 19 la kesi mpya za corona, na asilimia 26 ya vifo vilivyotokana na maradhi hayo ya kuambukiza katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Kufikia jana Alkhamisi, bara hilo lilikuwa limesajili zaidi ya kesi milioni 2.7 za virusi vya corona, mbali na vifo zaidi ya 64,000.
Nkesangasonga ameeleza bayana kuwa, bara la Afrika linahitaji chanjo za kukabiliana na Covid-19 hivi sasa, haswa kwa kuzingatia kuwa yumkini spishi mpya ya kirusi cha corona iliyoripotiwa nchini Afrika Kusini ikasambaa kwa kasi katika nchi nyingine za bara hilo.